吃瓜头条

Chuo Kikuu cha Kenyatta Chaadhimisha Siku ya Kiswahili Duniani

Chuo Kikuu cha Kenyatta kimeungana na jumuiya ya kimataifa kuadhimisha Siku ya Kiswahili Duniani, maadhimisho yanayotambua mchango wa lugha ya Kiswahili katika kuimarisha mawasiliano, elimu, utamaduni, ubunifu na maendeleo endelevu.
Maadhimisho ya mwaka huu yaliongozwa na kaulimbiu: “Kiswahili, uwezo wa wingi lugha na akili unde katika michezo na uhifadhi wa mazingira kwa maendeleo endelevu.” Kaulimbiu hiyo inaangazia nafasi ya Kiswahili katika kukuza ushirikishwaji, kuendeleza teknolojia na ubunifu, pamoja na kuhamasisha uhifadhi wa mazingira.
Wakizungumza wakati wa maadhimisho hayo, washiriki walisisitiza umuhimu wa Kiswahili kama lugha inayounganisha jamii, kuendeleza utafiti na maarifa, na kuchochea ushirikiano wa kitaifa na kimataifa. Pia walieleza kuwa matumizi ya Kiswahili katika elimu, sayansi, teknolojia na mawasiliano yana mchango mkubwa katika kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu.
Chuo Kikuu cha Kenyatta kinaendelea kuimarisha matumizi ya Kiswahili katika ufundishaji, utafiti, ubunifu na mawasiliano, kikithibitisha dhamira yake ya kukuza lugha hiyo kama nyenzo muhimu ya maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kiutamaduni nchini Kenya, barani Afrika na duniani.